ELIMU KWANZA

ELIMU KWANZA
KWETU FEDHA SIO KIPAUMBELE.

Wednesday, 6 November 2013

Faida 4 za kuwa na wivu kwa mumeo

ASSALAM Alaikum! Ni furaha yangu kwa mara nyingine tena kukutana nanyi kupitia safu hii ya Mashamsham nikiamini muwazima na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku.
Mpenzi msomaji wangu, utakumbuka wiki iliyopita nilizungumzia sababu za baadhi ya wake za watu kutembea na wapangaji wao au wenye nyumba. Ni mada iliyoonekana kuwavutia wengi, nadhani ni kwa sababu ni tabia inayoonekana kushamiri sana mtaani.
Kikubwa ni mume kuhakikisha anamuweka mbali mke wake na wanaume wakware ikiwa ni pamoja na kumpa somo la kuhakikisha anawaepuka wale wanaoonekana kuwa na dhamira ya kuwaharibia maisha yao ya ndoa.
Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita, sasa nirudi katika kile nilichodhamiria kukuandikia wiki hii. Hivi karibuni nilizungumza na mmoja wa wasomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina moja la Husna wa Arusha.
Yeye alinilalamikia kuhusu tabia ya mume wake kumjia juu kila anapohoji kuhusu kuwasiliana mara kwa mara na wanawake, tena nyakati za usiku.
“Yaani hakuna kitu ambacho kinaniuma kama ninaposikia mume wangu akiongea na mwanamke mwenzangu ambaye simjui. Kwa kifupi nina wivu sana kwa mume wangu na hii yote ni kwa sababu nampenda sana.
“Tatizo ni kwamba nikiuliza tu naishia matusi na siku hiyo anaweza kuondoka akarudi muda anaotaka. Hivi ni tatizo mie kuwa na wivu kwa mume wangu?” aliuliza Husna.
Kimsingi suala la kuwa na wivu kwa mpenzi wako ni jambo lisilokwepeka hasa kwa sababu kubwa ya kuaminika kwake kwamba ni moja ya kigezo cha kuonesha jinsi unavyompenda mpenzio.
Pia inaonesha ni jinsi gani hauko tayari kwa namna yoyote ‘kushea’ na mwingine. Ndiyo maana wanawake wengi hawataki kusikia suala la ukewenza kabisa licha ya kwamba jambo hilo limepewa baraka zote na dini au tamaduni zao.
Lakini kubwa katika wivu ni kutokuwa tayari kuona tunasalitiwa na wapenzi na hasa kwa wale tunaowapenda kiukweli kutoka mioyoni mwetu na zaidi ukute ndiyo tumeshawagharamikia kiasi cha kutosha na kujitoa kwao kwa kila kitu.
Niwaambie kitu wapenzi wasomaji wangu? Jamani kama ulikuwa hujui, mapenzi ni ‘full’ uchoyo, ‘full’ kujipendelea. Mpenzi mwanaume kwa mfano, anaweza kufikiria kwamba ni yeye tu anayestahili kumfanya mpenzi wake acheke na kufurahi.
Na akitokea mwanaume mwingine akapata nafasi ya kumfurahisha mpenzi huyo hata katika stori za kawaida tu, unaweza ukasikia akisema: “Hivi wewe una nini na huyo jamaa, mbona unamchekeachekea, au…!” Hiyo ndiyo choyo ya penzi.
Pamoja na ukweli kwamba tabia ya wivu inapozidi hugeuka kero, kabla hatujafika huko hebu tuangalie nafasi ya wivu katika mapenzi. Swali ni kwamba, je, wivu unatakiwa kuchukua nafasi katika maisha yetu ya kila siku?
Kwa wasiojua maana hasa ya wivu wanaweza kuishia kusema kuwa na wivu kwa mpenzi wako ni ushamba lakini nionavyo mimi wivu ukitumika vizuri unaleta faida na una nafasi muhimu katika mapenzi.
Ndiyo maana leo nimeamua kuainisha faida nne za mwanamke kuwa na wivu kwa mume wake kama ifuatavyo;
Kwanza, inaonesha jinsi gani unajali. Sote tunaamini pasipo na wivu hata chembe, hapana mapenzi ya kweli. Kumuonesha wivu mumeo ni kumjulisha ni kiasi gani unamjali na kumpenda na kwamba yeye ni mtu maalum sana kwako.
Jamani, mahali penye mapenzi yasiyo na wivu hata kidogo, panatia shaka na mara nyingi majibu yake ni kutokuwa ‘siriasi’ katika uhusiano au huenda kuna kupitisha muda tu na kwamba labda hakuna ‘future’.

Pili, wivu wa mke kwa mume ni ishara ya kulithamini penzi. Kwa mfano, mwanamke anaweza kumtumia mumewe ujumbe usemao:
“Siyo kama sikuamini dear, wivu wangu kwako ni katika kuuthamini uhusiano wetu, mimi na wewe ni umoja wenye thamani kubwa, tusiruhusu kuuchezea nje yetu.” Hii inaonesha maana na nafasi ya wivu katika uhusiano.

Tatu, wivu kwa wanandoa ni katika kukumbushana. Kauli na matendo yanayoashiria kumuonesha wivu mpenzio, vinasaidia kwa kiasi kikubwa kumfanya mwenzi wako asijisahau katika jukumu la kulienzi penzi lenu hata akiwa mbali ya upeo wa macho yako.

Nne, kwa namna moja au nyingine, wivu unaweza kukujengea heshima. Kwa mfano, mke mwenye wivu na mumewe hujijengea heshima ya kwamba kweli anamjali na kumpenda lakini pia anaweka mazingira ya kutosumbuliwa kwa mume wake huyo na kumjengea heshima yake kama mume wa mtu.

No comments:

Post a Comment